What REEL on Social Media
BBC :Mugabe ateuliwa kuwa mwenyekiti wa AU
Rais mkongwe wa Zimbabwe Robert Mugabe, mwenye umri wa miaka
tisini, sasa ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa muungano wa Afrika-AU.
Wajumbe walimteuwa Mugabe kwa kauli moja katika mkutano wa
AU unaoendelea mjini Addis Ababa-Ethiopia.
Uteuzi wa Mugabe kuongoza muungano huo mkubwa
ulio na wanachama zaidi ya arubaini, sasa umeingiza doa ndani ya AU, kwani
Mugabe hana uhusiano mzuri na mataifa ya Magharibi, hasa baada ya kukaa
uongozini tangu Zimbabwe ilipojipatia uhuru mnamo mwaka wa 80.
Saud Arabia yahairisha Viboko vya mwana Blogu
Mamlaka nchini Saudi Arabia kwa mara nyengine tena
imeahirisha adhabu nyengine ya viboko dhidi ya mwanablogu Raif Badawi.
Hakuna sababu iliotolewa,lakini awamu mbili za kutoa adhabu
kama hiyo hapo awali ziliahirishwa kutokana na sababu za kiafya.
Bwana Badawi amepewa hukumu ya viboko 1000 pamoja na
kuhudumia kifungo cha miaka 10 jela kwa kutusi Uislamu.
Mwanaharakati wa Saudia ambaye pia ni wakili Suad al
Shammary ambaye alifanya kazi na bwana Badawi katika blogi yake ameachiliwa
huru.
Alizuiliwa kwa miezi mitatu bila kufunguliwa mashtaka kuhusu
matamshi aliotoa katika mtandao wa Twitter ambayo wapinzani wake walisema
yanapinga Uislamu.
Aliyekuwa kiongozi wa makaburu aachiliwa
kiongozi wa zamani wa utawala wa kiimla wa makaburu nchini
Afrika Kusini na ambaye alikuwa kinara wa kuongoza kitengo hatari cha kuwatesa
watu weusi, Eugene de Kock, amesamehewa, kuhurumiwa na kuondolewa gerezani.
Eugene Alexander de KOCK alikuwa akitumikia hukumu ya
mauwaji na mateso kwa wakereketwa wengi wa chama cha ANC, lakini sasa waziri wa
haki na sheria Nchini Afrika Kusini, Michael Masutha, amesema kuwa de Kock
ameachiwa huru kwa manufaa ya umoja wa kitaifa.
Alikuwa ametubu mbele ya tume ya haki na maridhiano kwamba
alikuwa amesababisha zaidi ya vifo vya watu mia moja na pia kuhusika katika
vitendo vya kuwatesa watu kinyama na ufisadi, hasa akiwalenga waliokuwa
wakipinga utawala wa ubaguzi wa rangi.
Kanali huyo wa zamani wa polisi aliyekuwa na mataji mengi
mno alisamehewa kwa mengi ya makosa aliyofanya, lakini akazuiliwa gerezani kwa
makosa dhidi ya binadamu kabla ya kufungwa jela maisha.Tarehe ya kuachiwa huru
kwake kwa sasa bado ni siri.
CloudsFM
WASTARA ACHAGULIWA KUWA BALOZI WA KAMPENI YA NISAIDIE MIMI
SHILINGI 500 NIPATE ELIMU
Msanii wa Bongo Movie,Wastara Juma ameteuliwa kuwa balozi wa
kampeni YA ‘Nisaidie mimi Shilingi 500 nipate elimu’’ambayo inalenga kuwasaidia
watoto wa kike ambao wameshindwa kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali
ikiwemo kukosa ada ambapo kampeni hiyo itaanzia katika mkoa wa Morogoro.
Instagram
Kassim mganga:ndugu zangu tusiwasahau ndugu zetu walemavu
wana mengi na changamoto nyingi mno za kujadili na sisi, tuwawezeshe kwa namna
yoyote ile WANAWEZA #IjumaaKareem.Blog
Jeshi la Polisi wilayami Moshi mkoani Kilimanjaro
linamshikilia mwalimu mmoja wa shule ya sekondari kwa tuhuma za kumbaka
mwanafunzi wa kidato cha tatu.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Koka Moita
alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 11:45 katika chumba cha darasa
la maabara shuleni hapo.
Kamanda Moita alisema mwalimu huyo alimwita mwanafunzi huyo
katika chumba hicho na kuanza kumtomasa mwilini na baadaye alimvua nguo kwa
nguvu, kisha kumuingilia.
Ameongeza kuwa kutokana na maumivu aliyoyapata alipelekwa
Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi kwa matibabu. Kamanda Moita alisema mtuhumiwa huyo
anashikiliwa na jeshi la Polisi hivi sasa.
Saleh Jembe
NGASSA ASEMA ANAREJEA YANGA KWA AJILI YA KUAGA TU!
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Khalfan Ngassa, amesema
kuwa amerejea kundini kuitumikia timu hiyo kwa moyo mmoja lakini kubwa zaidi ni
kuwa anataka kuwaaga mashabiki wa Jangwani.
Tangu siku kumi zilizopita, Ngassa hakuonekana Jangwani huku
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Kiboroha akisikika akisema wamedokezwa kuwa staa
huyo amekwenda Afrika Kusini kufanya majaribio lakini Ngassa mwenyewe amesema
alitimkia Tanga kupumzisha akili kutokana na deni la shilingi milioni 45
analodaiwa na benki, ambalo amesusiwa na viongozi wa Yanga walilokubaliana
walilipe kwa pamoja.
Ngassa ameliambia gazeti la maarufu la michezo nchini
Tanzania la Championi kwamba amefikia maamuzi ya kurejea kwenye timu hiyo baada
ya familia yake kuahidi kumsaidia kulipa deni hilo lililotokana na kiungo huyo
kusaini Yanga akiwa ana mkataba na Simba.
Ngassa ambaye ameshajiunga na wenzake kambini Bagamoyo
kujiandaa na mechi dhidi ya Ndanda FC itakayopigwa keshokutwa Jumapili,
amesisitiza kuwa amepanga kujituma zaidi kuhakikisha Yanga inakuwa bingwa na
kufanya vizuri kwenye mechi zote.
“Leo (juzi Jumatano) nimeingia kambini huku Bagamoyo
nikiendelea na mazoezi kujiandaa na mechi ya ligi kuu dhidi ya Ndanda FC, hiyo
ni baada ya familia yangu kuahidi kunisaidia kulipa deni langu la benki.
“Tumefikia hatua hiyo baada ya viongozi (wa Yanga) kukiuka
makubaliano na kunisusia kulipa deni hilo, kiukweli akili yangu imerejea katika
hali ya kawaida, hivyo ninaahidi kuitumikia timu yangu kwa moyo kwa kufunga na
kutengeneza mabao kama njia ya kuwaaga mashabiki wa Yanga kutokana na mkataba
wangu kumalizika mwisho wa msimu huu.
“Kikubwa ninataka kuwaonyeshea hao wanaozusha kuwa kiwango
changu kinashuka kutokana na starehe na wanawake hao watatu wanaozusha nimewaoa
wakati nina mke wangu mmoja wa ndoa,” alisema Ngassa
TAMBWE: BADO HATUJAFIKIA KIWANGOTUNACHOTAKA NA HATUJAKATA TAMAA
Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe amesema licha ya
kutofanya vizuri katika kiwango anachotaka yeye na wenzake, wamekuwa
wakiendelea kujituma tu.
Tambwe amesema wamekuwa wakijituma kwa juhudi kubwa huku
wakiamini mambo yatabadilika kama hawatakata tamaa.
“Unajua ukiendelea kujituma, hata kama hayaendi vizuri
baadaye yanaweza kubadilika na ukafanya vizuri.
“Kitu kizuri mimi na wenzangu hatukati tamaa, hata ukija
mazoezini utaona watu wanavyojituma na tuna imani siku itafika tuanze kufanya
vizuri,” alisema Tambwe.
Mbeyayetu:
TRA MBEYA WAWEKWA KITIMOTO NA WAFANYABIASHARA,
WASHINDWA KUTOA MAJIBU WAKATAA KULIPA ONGEZEKO LA KODI
WAFANYABIASHARA wa Jiji la Mbeya walifunga maduka yao
wakipinga kulipa mabadiliko ya sheria ya kodi ya 2014, ambayo walidai kuwa
imeongeza ututiri wa kodi na kuendelea kuwakamua.
Wakizungumza baada ya kukutana katika mkutano wao
uliofanyika ndani ya ukumbi wa Mkapa, Jijini hapa, ulioshirikisha watendaji wa
Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Mkoa wa Mbeya na jeshi la polisi,
wafanyabiashara hao walisema kodi hiyo hailipiki na hawako tayari kulipa.
Awali baadhi ya wafanyabiashara walitoa malalamiko yao
mbalimbali kuhusu suaala la sheria mpya ya kodi ya mwaka 2014 kuwa inaongeza
kero kubwa kwa wafanyabiashara na itasababisha kukwamisha ustawi wao.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Masaga Salum, alisema
mabadiliko hayo ya sheria ya kodi hayawatendei haki wafanyabiashara kwa kuwa
hawakushirikishwa katika mchakato wa kuandaliwa kwa sheria hiyo.
“Haiwezekani serikali ikawa inatoa misamaha ya kodi kwa
wawekezaji wakubwa toka nje ya nchi , huku ikitumia nguvu kubwa ya ukusanyaji
wa kodi kwa wafanyabiashara wadogo wa hapa nchini ambao ndio wapiga kura
wanaowaweka madarakani ”
No comments:
Post a Comment